edu34

South Eastern Bible College

Chuo cha Biblia Mtama kinachojulikana sasa kama South–Eastern Bible College kipo Kanda ya Kusini Mashariki.  Chuo kilianza kama Chuo cha Kupanda Makanisa. Lengo kuu likiwa ni kuwaandaa watumishi wenyeji kwa ajili ya kuanzisha makanisa katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Maono ya kuanzisha chuo hiki yalianza na Makamu Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God, Mchungaji Daktari Magnus Mhiche ambaye kwa wakati ule alikuwa Askofu wa Jimbo la Mashariki. Darasa la kwanza lilianza kule Masasi kwa mchungaji Patrick Challu tarehe 11 Julai 2005 chini ya usimamizi wa Mchungaji Isaac Njara.

Kutokana na uhitaji mkubwa wa watumishi wa Mungu katika mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara, ilionekana kuna umuhimu wa kuwa na eneo kubwa ili kuweza kujenga Chuo na kuanzisha miradi mbalimbali ili kuigusa jamii ya Lindi na Mtwara. Mnamo tarehe 31 Mei 2006 eneo lilinunuliwa lenye ukubwa wa ekari 72.5. Ekari 6 zilitolewa kwa Matumizi ya Chuo cha Ufundi na 66.5 kwa ajili ya South Eastern Bible College. Ujenzi ulianza mwaka huo huo.

Tarehe 21 Julai 2008 ujenzi ulikamilika na Chuo cha Kupanda Makanisa kilihamishwa kwenda Mtama, Lindi kutoka Masasi. Mwaka 2009, uongozi wa Kanisa chini ya Askofu Mkuu Daktari Barnabas Mtokambali ulikibadilisha Chuo kuwa Chuo kinachotoa stashahada ya Biblia na Huduma za Kanisa kwa miaka mitatu. Hivyo tarehe 4 Januari 2010, chuo kilianza kutoa mafunzo ya stashahada.

Mchungaji Isaac Njara alihamishwa kwenda Chuo cha Biblia Mbeya na Mchungaji Richard Mmary aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo wa kwanza wa Mtama Bible College ambacho kwa sasa kinaitwa South–Eastern Bibe College.

edu35

Dr. Magnus Mhiche, Mwanzilishi wa maono ya chuo cha Mtama

edu36

Majengo ya chuo cha South Eastern Bible College

Chuo kilianza kikiwa na walimu wawili tu ambao ni mchungaji Richard Joel Mmary, na Mchungaji Exaud Lisulile aliyeteuliwa kuwa mwalimu wa taaluma, meneja shughuli na mhasibu. Wachungaji Mmary na Lisulile walifanya kazi kubwa kuhakikisha chuo kinastawi na kutimiza kusudi la kuanzishwa kwake. 

Mnamo Januari 2013, Mchungaji Isaac Edward Challo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo badala ya Mchungaji Richard Joeli Mmari ambaye alihamishwa kwenda Central Bible College Dodoma kuanza masomo ya uzamili. Watumishi 210 wamehitimu na kwenda katika huduma tangu Chuo Kimeanza.  Chuo kimendelea kustawi na kuongezeka wanachuo kutoka Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dar-Es-salaam, Ruvuma na mikoa wenyeji ya Lindi na Mtwara. Kwa sasa chuo kina walimu 4 na wanafunzi 129.