edu21

Southern Bible College

Chuo cha Biblia Mbeya ambacho kwa sasa kinaitwa Southern Bible College ndicho chuo cha kwanza kuanzishwa katika kanisa la Tanzania Assemblies of God. Kilianzishwa na Mmishenari Wesley Hurst mwaka 1954. Mmishenari Hurst alifika Mbeya tarehe 14/6/1952 akitokea Marekani ili kusaidia kazi ya kuendeleza uamsho mkubwa ambao ulikuwa umepamba moto kule kusini mwa Tanzania. Mmishenari Hurst alitumwa toka makao makuu ya Assemblies of God Marekani baada ya Mmishenari Ragner Udd kuomba aletwe mmishenari wa kumsaidia huduma ya kuandaa watumishi. 

Wamishenari Udd na Hurst wakisaidiana na Mchungaji Moses Kameta, walitafuta eneo la ardhi kwa ajili ya kujenga Chuo. Walifanikiwa kupata eneo lenye ukubwa wa ekari 20, ambalo walipewa na kiongozi wa kimila wa kabila la Wasafwa, Chifu Mwalyego wa Utengule. Eneo hilo lipo katika Kata ya Kalobe karibu na kijiji cha Itende, kilometa mbili na nusu kutoka barabara kuu iendayo Tunduma. Sehemu kubwa ya ardhi hiyo ilitaifishwa na serikali baada ya Azimio la Arusha na kubaki ekari saba na nusu.

Mmishenari Wesley Hurst alianza kutekeleza maono ya kuwa na Chuo cha Biblia mnamo 1952 kwa kusimika mahema ambayo yalitumika kama madarasa ya shule ya msingi na ya mafunzo ya elimu ya Biblia kwa wachungaji. Mwaka 1953 alianza kujenga mabweni kwa ajili ya Chuo cha Biblia. Baada ya kumaliza ujenzi wa mabweni mwaka 1954, Chuo kilifunguliwa rasmi na Mmishenari Hurst akawa Mkuu wa Chuo wa kwanza.

Walimu wa kwanza katika chuo hicho walikuwa ni Wamishenari na wake zao. Mchungaji Moses Kameta aliwasaidia kutafsiri, kwa sababu lugha iliyotumika kufundishia ilikuwa ni Kinyakyusa. Kusudi la chuo hiki lilikuwa ni kuwaandaa watumishi wazawa wa Tanganyika kwa ajili ya huduma. Chuo kilipoanza kilijulikana kwa jina la Maranatha Bible College jina hilo lilibadilishwa na kuwa Tanganyika Bible Institute. Baadaye chuo kilibadilishwa jina tena na kuitwa International Bible College. Jina hili halikudumu maana baadaye ilipendekezwa kiitwe Mbeya Bible College. Sasa chini ya Mpango Mkakati kinajulikana kama Southern Bible College.

edu22

Mwonekano wa Chuo cha Mbeya kati ya mwaka 1958 na 1959

edu23

Mmishenari Weslay Hurst na Mke wake mkuu wa Chuo wa Kwanza

Chuo hiki kina mchango mkubwa sana katika kukua kwa Kanisa la Tanzania Assemblies of God. Miongoni mwa wanafunzi wa kwanza waliosajiliwa kusoma ni Mchungaji Yohana Mpayo, Mchungaji Ramsey Mwambipile, Mchungaji David Mwainyekule na Mchungaji Asajigwe Mwaisabila. Wachungaji hao walikuwa kichocheo kikubwa kwa uamsho wa kwanza katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God.

Chuo kiliendelea kukua kutoka kusajili wanafunzi 6 kwa mwaka kilipoanzishwa hadi wanafunzi 211 kwa mwaka ilipofika mwaka 2018.  Tangu Chuo kuanzishwa, zaidi ya wanafunzi 3,592 wameshahitimu. Wanafunzi hao walitoka sehemu mbali mbali za nchi ya Tanzania na nchi za jirani kama Rwanda, Burundi na DRC Congo.

Majengo zaidi yamejengwa ili kukidhi hitaji la ongezeko la wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa Chuo.  Mengi ya majengo hayo yalijengwa na Wamishenari kwa nyakati tofauti katika historia ya Chuo. Wamishenari wanaokumbukwa ni pamoja na James Farrer, Delmer Kingsrighter, Bailey Rogers na John Ford.  Baadaye bweni kubwa la ghorofa, jengo la ibada, ukumbi wa chakula na madarasa mawili yalijengwa kwa ufadhili wa Mchungaji Randy Hurst ambaye ni mtoto wa Mmishenari Wesley Hurst. Mmishenari Wesley Hurst alimaliza huduma yake hapa Tanzania mwaka 1960.

Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea tovuti ya chuo cha Southern Bible College kwa kubofya kitufe hapo chini