Northern Bible College

Chuo cha pili kilikuwa ni Chuo cha Biblia Arusha ambacho kilianzishwa mwaka 1958 ili kuyafikia maeneo ya Kaskazini. Kwa sasa Chuo hicho kinajulikana kama Northern Bible College. Wamishenari wa Assemblies of God waliokuweko Tanganyika wakati huo waliamua kuwekeza nguvu zao kwenye kuanzisha makanisa na Chuo cha Biblia katika Ukanda wa Kaskazini mwanzoni mwa miaka ya 1950. Northern Bible College kilianzishwa na Mmishenari Paul Bruton ambaye ni miongoni mwa Wamishenari wa kwanza waliotumia muda wao mwingi kuhubiri Injili katika ukanda ule wa Kaskazini.

Mmishenari Bruton baada ya kuona vijana wengi wanaokoka na kuitikia wito wa kumtumikia Mungu aliamua kuweka makao yake Arusha. Mwaka 1958, Mmishenari Bruton alipatana na mkulima mmoja wa Kimarekani aliyekuwa na mashamba Arusha ili ampatie ardhi ya kujenga Chuo. Alifanikiwa kupata takribani ekari 10 kwa ajili ya kusudi hilo katika eneo lililo pembezoni mwa mto Ngaramtoni.

Mmishenari Bruton alianza ujenzi wa Chuo kwa kujenga majengo matano ambayo kati ya hayo manne yalitumika kama mabweni na moja lilikuwa na vyumba viwili vya madarasa na ukumbi wa ibada. Chuo kilianza rasmi Aprili 1959 kikiwa na wanafunzi 16. Mmishenari Bruton alikuwa ndiye mwalimu na Mkuu wa Chuo wa kwanza. Walimu wengine wa mwanzoni waliosaidia kufundisha ni Wamishenari Stephen Van der Merwe, Marvin Thomas, na Griffins. Walimu wazawa walikuwa Yohana Mpayo, Petros Lwesya, na Peter Bundala.

Miongoni mwa wanafunzi wa kwanza wa Northern Bible College ni Mchungaji Steven Kitulika ambaye aliwahi kuchunga Kanisa la Calvary Temple Arusha; Mchungaji Wilson Kimaro wa TAG Calvary Temple Arusha; Moses Cornelius wa Dodoma; Mchungaji Jason Lugwisha alikuwa mchungaji wa Kanisa la TAG Kirumba Mwanza; Mchungaji Simon Mallya aliwahi kuchunga Kanisa la Temeke; Mchungaji William Magilali aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa la Nzega, na mchungaji Lusito.

edu24
edu25

Mmishenari Paul Brutoni na Mke wake Mkuu wa chuo wa kwanza

edu26

Jengo la Bweni la Chuo

Kwa sababu ya matatizo mbalimbali chuo kilifungwa kwa miaka kadhaa tangu mwaka 1961 kabla hata ya kufanyika kwa mahafali ya kwanza iliyokusudiwa mwaka huo.  

Chuo kilirudia tena utendaji wake mnamo mwaka 1967 chini ya Mmishenari Jerry Spain na mke wake ambao walitumwa toka Marekani kwa kusudi la kukifungua tena chuo hicho. Mmishenari Spain alipotembelea Arusha alisema enzi za uongozi wake fedha ilikuwa ni shida sana kupatikana. Hivyo ilibidi ada ya wanafunzi ithaminiwe kwa kutumia debe la unga wa mahindi na maharage.

Wamishenari walioungana na Mmishenari Spain kufundisha Arusha Bible College ambacho kwa sasa kinaitwa Northern Bible College ni Sandra Goodwin (Mwaka 1971); Mike McClaffin na mke wake Linda McClaffin (1973); na Charles Petroskys ambaye alifundisha kama mwalimu wa muda. Kwa sababu zilizokuwa juu ya uwezo wa Kanisa kwa wakati huo Chuo kilifungwa tena kati ya mwaka 1979 na 1982 wakati ambapo Mmishenari Spain na walimu wote walihama na kwenda kuanzisha chuo kipya Nairobi kilichojulikana kwa jina la EAST.

Mchungaji Emanuel Laizer aliteuliwa na uongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God kwenda kusimamia Kanisa na mali za Chuo. Wakati akiendelea kusimamia Wamishenari wakataka kukiuza chuo baada ya kuuza baadhi ya vifaa vyake kwa chuo cha Baptist kilichoko karibu na Ngaramtoni ambacho kwa sasa kinaitwa Mount Meru University. Ndipo mchungaji akafunga safari kumwendea mchungaji Joshua Ngataiti na kumwambia kwa nini unalala? Amka chuo kinauzwa! Mchungaji Laizer na mchungaji Joshua Ngataiti walielekea Ngaramtoni na kuamua kupanda miti na migomba kwenye eneo la chuo usiku kucha ili kukinusuru chuo.

Wamishenari walipotaka kuuza walisema, “hii ni mali yetu na Kanisa la Ngaramtoni, mtu akitaka kununua Chuo basi na atununue na sisi”, na hivyo wanunuzi wakakosa nguvu. Kisha mchungaji Laizer akaingia kwenye maombi ya kufunga wiki moja kumuuliza Mungu kuhusu hatima ya Chuo. Mungu akamjibu kuwa “Chuo kitaendelea na nitakibariki na kitakuwa Chuo kikubwa kwa vizazi vijavyo.”

Kisha Mungu akamuuliza “Wewe utatoa nini ili kusaidia Chuo kianze?” Mchungaji Laizer akajibu kuwa “Nitatoa ndama na chakula cha kuanzia.” Na hivyo ndivyo alivyofanya na kuwezesha Chuo kufunguliwa tena mwaka 1982. Mwaka huo huo mchungaji Laizer akaugua na kufariki, na mchungaji Peter Mitimingi akapewa kukiongoza Chuo kwa nafasi ya Mkuu wa Chuo. Ingawa changamoto mbalimbali zilijitokeza kuanzia hapo, Mungu alisimamia Neno lake na hata sasa Chuo kinaendelea kusonga mbele.

Zaidi ya watumishi 1,200 wamehitimu na kuingia shambani mwa Bwana tangu kuanzishwa kwake. Tunazo kila sababu za kumtukuza Mungu kwa mchango mkubwa wa Chuo hiki katika kulikuza Kanisa la Bwana wetu Yesu Kristo.

Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea tovuti ya chuo cha Northern Bible College kwa kubofya kitufe hapo chini