edu31

Lake Victoria Bible College

Historia ya kuanzishwa kwa Chuo cha Biblia Mwanza, ambacho kwa sasa kinajulikana kama Lake Victoria Bible College, ni tofauti kidogo na jinsi Vyuo vingine hapo juu vilivyoanzishwa. Mwanzilishi wa Chuo hiki hakuwa na mpango wa kujenga Chuo cha Biblia, bali alikusudia kujenga kituo ambacho kingekuwa kitega uchumi cha kulisaidia Kanisa kupata fedha za kutimiza malengo yake.

Mmishenari Jim Petersen aliyekuwepo Mwanza mwaka 1994 alinunua eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mikutano. Mradi huo hapo ulipoanza uliitwa, “The Mwanza Project” ambao baada ya kukamilika kwake ungekabidhiwa kwa Kanisa la Tanzania Assemblies of God kama mradi wa kanisa kwa ajili ya kukodisha kwa matumizi ya mikutano na semina mbali mbali ili kanisa liweze kujipatia kipato.

Hivyo ununuzi wa kiwanja ulipokamilika ujenzi ulianza chini ya usimamizi wa ndugu Suleiman Seni. Ujenzi wa kituo kile haukuweza kukamilika kwa sababu mwaka 1997 Mmishenari Jim Petersen alihamia Zambia. Hadi wakati anahama, majengo aliyokwisha kujenga ambayo hayakukamilika ni nyumba moja ya kuishi, ukumbi wa mikutano, ofisi, vyoo na bwalo la chakula.

Baada ya kuondoka Mmishenari Petersen, mwaka huo huo Mmishenari mwingine aliyeitwa Tim Jarvis alifika Mwanza na kuuendeleza mradi ule kwa kukamilisha baadhi ya majengo ambayo mtangulizi wake hakuyamaliza. Baada ya kumaliza kazi yake, Mmishenari Jarvis aliamua kukabidhi kituo hicho kwa uongozi wa Tanzania Assemblies of God.

edu33

Mmishenari Tim Jarvis na familia yake

edu32

Majengo ya kwanza ya Lake Victoria Bible College

Mwaka 1999 aliyekuwa Askofu Mkuu Mchungaji Ranwell Mwenisongole na Katibu Mkuu Mchungaji Yusufu Mbelwa walienda Mwanza ili kukabidhiwa majengo ya kituo hicho. Walipoyaona majengo hayo, waligundua kuwa hayakukamilika kulingana na michoro. Walivunjika moyo kwa kuwa Kanisa halikuwa na fedha za kukamilisha ujenzi huo. Hivyo, viongozi hao hawakuwa tayari kupokea majengo hayo yasiyokamilika kwa maana wasingeweza kuyatumia katika hali hiyo kwa mradi uliokusudiwa.

 Kati ya mwezi Aprili na Mei 2000, Mkuu wa Wamishenari Afrika Mashariki, Jerry Spain, alitembelea Mwanza na kufika eneo la “Mwanza Project.” Alipokuwa akijadiliana na Wamishenari wenzake alioongozana nao juu ya nini kifanyike kuhusu majengo yale huku wakibubujika machozi, ndipo alipotamka, “Mahali hapa hapatajengwa kituo cha mikutano, bali kituo cha kujifunzia na kuandaa wachungaji katika ukanda huu.” Kisha wakamwomba Mungu ili awaongoze kufanya maamuzi kuhusu hatma ya mradi ule.

Majuma machache baada ya wamishenari kuomba uongozi wa Mungu, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Taifa wakati huo, Mchungaji Jotham Mwakimage, aliwasiliana na Mmishenari Jarvis ili aweze kutembelea kituo kile. Mkurugenzi Mwakimage alipokiona kituo hicho, alifurahi na kutamka kuwa Idara ya Elimu itakitumia kama Chuo cha Biblia.

Mchungaji Mwakimage aliporudi Dar es Salaam, aliijulisha Ofisi Kuu kuwa mahali pale panafaa kuwa Chuo cha Biblia. Kibali kikatolewa cha kuanza Chuo, na mara moja maandalizi ya kuanza Chuo yakaanza. Mwaka huo huo wa 2000 akaletwa Mkuu wa Chuo wa kwanza Mchungaji Ronald Swai na Msajili wa Chuo, Rebeka Kakila kutoka Chuo cha Biblia Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya kuanza masomo mnamo mwaka 2001. Mchungaji Ronald Swai na Rebeka Kakila ndio walimu wa kwanza wa Chuo cha Biblia Mwanza wakisaidiana na mama Joyce Jarvis.

Chuo kilifunguliwa na kuanza masomo rasmi mwezi Januari 2001 kikiwa na wanafunzi 33. Kwa kuwa hapakuwa na mabweni ya kulala wakati huo, wanafunzi walilala katika vyumba vilivyokuwa pembeni mwa ukumbi wa mikutano. Ukumbi huo wa mikutano ulitumika kama darasa.

 

Mwezi Machi 2001, ujenzi wa madarasa ulianza na kukamilika mwezi Mei chini ya usimamizi wa Mchungaji Ronald Swai. Kukamilika kwa madarasa kuliwezesha Chuo kuzinduliwa rasmi tarehe 8 Juni, 2001. Uzinduzi wa Chuo uliongozwa na aliyekuwa Askofu Mkuu, Mchungaji Ranwell Mwenisongole akiambatana na Makamu Askofu Mkuu, Mchungaji Rogathe Swai; Katibu Mkuu, Mchungaji Yusuph Mbelwa; na Mkurugenzi wa Elimu Mchungaji Jotham Mwakimage. Pia ulihudhuriwa na Mmishenari Jim Petersen na mke wake kutoka Zambia na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ndugu Steven Mashishanga.

Chuo kimeendelea kuimarika na kufikia wakati huu jumla ya watumishi 576 wamehitimu na kuingia kwenye huduma.

Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea tovuti ya chuo cha Lake Victoria Bible College kwa kubofya kitufe hapo chini