Global University Tanzania

Mwaka 1967 taasisi ya kujisomea iliyojulikana kama International Correspondence Institute (ICI) iliundwa chini ya Idara ya umisheni wa nje ya Assemblies of God huko Marekani. Lengo lilikuwa ni kutoa mafunzo ya masomo ya uanafunzi, uinjilisti, watendakazi pamoja na shahada ya kwanza kwa wanafunzi kote ulimwenguni. ICI ilibadilishwa na kuwa Chuo Kikuu kilichojulikana kama ICI University. Mwaka 2000 taasisi nyingine iitwayo Berean University iliungana na ICI Univesity kuwa Global University. 

Global University ilianza rasmi Tanzania mwaka 1972 ikiwa bado inajulikana kama ICI. Iliongozwa na Mmishenari Robert Cobb akishirikiana na Mchungaji David Mwakajinga wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Buguruni. ICI ilianzia kwenye makazi ya wamishenari yaliyoko eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam alikokuwa anaishi Mmishenari Cobb. Mwanzoni kabisa programu ya ICI ilijikita zaidi katika masomo ya Uinjilisti yaliyokuwa yanaitwa “Maswali Makuu ya Maisha.”

Kutoka nyumbani kwa Mmishenari Cobb, ofisi ya ICI ilihamia kwenye jengo walilojenga pembeni mwa Kanisa la TAG Kinondoni. Baada ya kuona mafanikio ya mpango huo, Mmishenari Cobb alianza kusimamia masomo ya shahada ya kwanza kwa njia ya kujisomea nyumbani.

Mmishenari Cobb alikwenda nyumbani kwao Marekani kwa likizo ya muda mrefu. Kwa kipindi alichokuwa likizo masomo ya ICI yaliendelea kusimamiwa na Wamishenari Bracy Greer, Kenneth Alba, na Timothy. Kufuatia usimamizi wa Mmishenari Timothy, Mmishenari Cobb alirudi na kuendelea na huduma yake ya kutoa mafunzo ya ICI.

Baada ya Mmishenari Cobb, Mmishenari Kenneth Moeckel aliteuliwa kusimamia ICI Tanzania. Wakati wa uongozi wa Mmishenari Moeckel, ofisi ya ICI ilihamia Dodoma kwa sababu yeye pia alikuwa Mkuu wa Chuo cha Biblia cha Assemblies of God Dodoma. Mmishenari Moeckel aliongoza ICI Tanzania kati ya mwaka 1982 na 1983. Wamishenari Bracy Greer, Mark Flattery na Kenneth Alba waliongoza ICI kwa nyakati tofauti kati ya 1984 na 1986. Mwaka 1987 ICI Tanzania iliongozwa na Mmishenari Larry Stevens ambaye alikuwa pia Mkuu wa Chuo. Mmishenari wa mwisho kuiongoza ICI alikuwa ni Dave Thompson. Aliteuliwa kuiongoza ICI kwa muda mfupi akiwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha AGBC Dodoma.

edu37

Mchungaji Gregory Malonnga

Mkurugenzi 1998 - 2003
edu5

Mchungaji Joyce Musembe

Mkurugenzi 2015 - sasa

Mwaka 1998, Wamishenari walikabidhi ICI kwa Kanisa la Tanzania Assemblies of God. Mchungaji Gregory Mallonga aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya Tanzania Assemblies of God kuwa Mkurugenzi wa kwanza Mtanzania wa ICI mwezi Agosti, 1998. Wakati wa uongozi wa Mchungaji Mallonga ofisi ya ICI ilirudi Dar es Salaam. Mchungaji Mallonga aliongoza ICI hadi mwaka 2003. Ni katika kipindi hiki cha uongozi wa Mchungaji Mallonga ICI ilibadilika kuwa Global University. Mwaka 2004 Mchungaji Dr. Jackson Nyanda aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Global University. Kwa kuwa Dr. Nyanda alikuwa mwalimu na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Dodoma, ofisi ilihamia tena Dodoma. Dr. Nyanda aliongoza Global University hadi 2008.

Mwaka 2009, Mchungaji Ezekiel Mwakajwanga aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Global University na ofisi ikarudi Dar es Salaam kwenye jengo la Makao Makuu ya Tanzania Assemblies of God. Mchungaji Mwakajwanga aliongoza hadi mwaka 2012.

Mwaka 2013 Mchungaji Dr. Geofrey Peter Majule aliteuliwa kuwa Mkurugenzi. Aliongoza kwa muda wa mwaka mmoja. Mwanzoni mwa mwaka 2014 Mchungaji Majule alirudishwa Dodoma kuendelea na huduma ya kufundisha chuoni na huduma za Global University zilisimamiwa na Idara ya Elimu Makao Makuu chini ya Katibu wa Idara ndugu Tadei Mbuta akisaidiwa na Mrs Emiliana Kalinga. Mwaka 2015 Mchungaji Joyce Musembe aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Global University hadi sasa

Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea tovuti ya Global University Tanzania kwa kubofya kitufe hapo chini