Global Harvest Bible College

Global Harvest Bible College ndiyo chuo pekee cha kutwa cha Tanzania Assemblies of God. Chuo kilifunguliwa na kuanza mafunzo mwezi Januari 2009. Uzinduzi rasmi ulifanywa na Rais wa Global University kutoka Marekani Dr. Garry Seevers tarehe 26 Aprili, 2009. Lengo la kuanzishwa kwa Chuo hiki ni kukidhi hitaji la mafunzo kwa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa mingine ya Tanzania, na hata kutoka nje ya Tanzania, wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo na hasa ya Kipentekoste tunayokubaliana kiimani.

Chuo hiki kina mikondo miwili ya mafunzo, yaani madarasa ya asubuhi na madarasa ya jioni. Madarasa ya jioni yanalenga kuwahudumia watu ambao ratiba za shughuli zao za kila siku haziwaruhusu kusoma muda wa asubuhi.

Chuo kinatoa mafunzo yake kwenye jengo la Makao Makuu ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God liliko Ubungo. Kilianza na wanafunzi 17 wa kutwa na 11 wa jioni. Global Harvest Bible College kinatoa mafunzo ya shahada ya kwanza ya Biblia na Teolojia, Elimu ya Kikristo, na Umisheni. Kwa sasa Chuo kina jumla ya wanafunzi 90 ambao kati yao wanafunzi 40 wa kutwa na 50 wa jioni.

Mkuu wa Chuo wa kwanza ni Mchungaji Ezekiel Mwakajwanga ambaye anaendelea hadi sasa. Walimu wa muda wote ni Dr. Immaculate Nhigula, Mwalimu wa Taaluma na Msajili; Mchungaji Isaac Challo, Mlezi wa Wanafunzi na Mchungaji Willimina Muimbula, Meneja Shughuli. Walimu wa muda mfupi ni: Mchungaji Joyce Musembe, Mchungaji Brayson Muimbula, Mchungaji Isaac Jeremiah, Mchungaji Rodgers Namwenje na Mchungaji Musa Ludengh’emya. Walimu wengine waliowahi kufundisha Global Harvest Bible College ni Wachungaji Gregory Mallonga, Samwel Mwaluvanda, Dr. Gerald Ole-Nguyaine, Grant Mwakasege, na Medard ByaMungu.

edu19

Mchungaji Ezekiel Mwakajwanga

Mkuu wa Chuo wa kwanza (2009 - sasa)

Kwa kuwa Global Harvest Bible College ni Chuo cha kutwa, kiliwalenga zaidi wanafunzi walioishi Dar-es-salaam. Hata hivyo baada ya muda mfupi, kilianza kupokea wanafunzi kutoka nje ya Dar-es-Salaam na hata nje ya nchi. Wanafunzi hao walijitafutia mahali pa kuishi kwa kujitegemea au kutegemezwa na makanisa rafiki. Chuo kimeshapokea wanafunzi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Msumbiji, Zimbabwe na DRC. Katika kutimiza lengo hili, Global Harvest imefanikiwa kudahili wanafunzi 216 wa ngazi ya shahada ya kwanza kwa kipindi chote cha miaka kumi ya Mpango Mkakati. Miongoni mwao, wanafunzi 84 wamehitimu hadi kufikia November 2018.