Central Bible College

Mwaka 1980 Chuo cha Dodoma ambacho kipo katikati ya nchi kilianzishwa ili kufikia Kanda ya kati na Magharibi ya nchi kwa urahisi zaidi.  Maono na malengo ya kuanzishwa kwake yalikuwa ni zaidi ya kufikia kanda hizo. Mwanzilishi wa Chuo cha Biblia Dodoma ni Wamishenari Ralph na Shirley Hagemeier. Kwa sasa kinaitwa Central Bible College. Mmishenari Hagemeier alifika Tanzania tarehe 21 Mei, 1967 akitokea nchini Marekani. Alipoingia nchini alijiunga na Chuo cha mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa muda wa miezi mitatu huko Mbeya. Baada ya kumaliza masomo ya lugha Mmishenari Hagemeier alikwenda kufanya huduma mjini Dodoma mwezi Januari 1968.  Mmishenari Hagemeier alikuwa Mmishenari wa nne kuja Dodoma baada ya Paul Bruton, Jimmy Beggs, na Morris Williams, almaarufu “Bwana Tembo.”

Mmishenari Hagemeier alianza kuhubiri katika makanisa mbalimbali yaliyokuwepo Dodoma wakati huo. Mnamo mwaka 1969 Mmishenari Hagemeier alitamani kulifanya Kanisa la Swaswa kuwa kituo cha mafunzo. Ndipo mwaka 1970 wakiwa na mmishenari Jimmy Beggs katika safari zao za kawaida wakapita eneo hilo la Miyuji na walipoliona yeye akavutiwa sana na eneo hili. Akaenda kuonana na uongozi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ili kuomba apewe eneo hilo kwa matumizi ya shughuli za kanisa.

Alikutana na changamoto mbalimbali katika kupata eneo hilo. Lakini aliendelea kuomba, wakati mwingine akilizunguka eneo hilo kwa imani na kukiri ahadi ya Maandiko kwamba patakapokanyaga miguu yetu Bwana atatupa kumiliki (Yoshua 1:3). Hatimaye mwaka 1976, Mtendaji Mkuu wa CDA wa wakati huo, Sir George Kahama, alikubali kumpatia Mmishenari Hagemeier eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 31.

Baada ya kupata uwanja huu Mmishenari Hagemeier aliamua kuhama kutoka Swaswa kwenda Miyuji akiwa na nia ya kuanzisha taasisi ya Mafunzo ya Kimataifa (International Training Institute). Nia yake ilikuwa ni kuwaandaa watumishi walioitwa kwa ajili ya huduma toka mataifa mbalimbali.  Mmishenari Hagemeier aliomba kibali cha ujenzi na serikali ilimruhusu kujenga.

Walioshiriki kufyeka pori ni Watson Nyirenda, William Manyerezi, Mzee Chilewa, Eliya Ngobito na Mzee Chigwasi. Mchungaji Eliya Ngobito alimsaidia sana Mmishenari Hagemeier kufyeka na kuandaa mazingira ya ujenzi wa chuo. Mmishenari Hagemeier alijenga nyumba ya kwanza ya tope kwa ajili ya mchungaji Ngobito na familia yake ili kulinda eneo la Chuo. Wakati zoezi la ufyekaji likiendelea, Mmisionari Hagemeier alisafiri kwenda Marekani ili kutafuta wahisani watakaoweza kusaidia kutekeleza maono hayo kifedha, vifaa vya ujenzi, na nguvu kazi watu.

Mmishenari Hagemeier akiwa Marekani, baadhi ya viongozi wa serikali ya Tanzania walimtaka Mchungaji Ngobito atoke katika eneo hilo wakihofia usalama wake kwa sababu ya hatari ya wanyama wakali na majambazi. Lakini Mchungaji Ngobito hakukubaliana nao, aliendelea kuishi hapo kwa imani.

Hatimaye, Mmishenari Hagemeier alirudi kutoka Marekani na ujenzi wa madarasa na mabweni ulianza mwaka 1978.  Wanafunzi wa kwanza hamsini wa Chuo cha Kimataifa cha Dodoma walisajiliwa mwaka 1980. Wanafunzi hao walitoka Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Rwanda. Pamoja na kwamba Chuo kilianza na mwanzo mgumu na mdogo, tunamshukuru Mungu kwamba kimepiga hatua kubwa kimaendeleo na kuna matumaini makubwa ya maendeleo zaidi huko mbeleni.

Walimu wa kwanza kabisa kufundisha walikuwa ni Wamishenari Ralph na Shirley Hagemeier na Mchungaji Eliya Ngobito. Mchungaji Ngobito alikuwa Mlezi wa wanafunzi. Baadaye Mchungaji Yohana Mahene alijiunga na timu ya walimu hao.

Kati ya wanafunzi hamsini wa kwanza kusajiliwa, waliohitimu ni 21. Pamoja na mambo mengine, hali hiyo ilisababishwa na mgogoro uliopelekea Kanisa kugawanyika na kuzaliwa kwa EAGT. Mahafali ya kwanza ya Chuo cha Kimataifa Dodoma yalifanyika mwezi Disemba mwaka 1982. Wahitimu wa kwanza wa stashahada ni: Bartholomew Sanga, Christina Kaligilwa (Christina Gatabazi), Charles Ndonya, Jacob Kayombo, Lazaro Ngendera, Nathanael Sasali, Ranwell Mwenisongole, Tryphone Tibilole, Yohana Kisukuli, na Paulo Mfyomi.

Mwaka 1983, Chuo kilifungwa kwa sababu ya mgogoro wa kiuongozi uliosababisha mpasuko mkubwa wa Kanisa. Mgogoro huo ulianza baada tu ya kumalizika Mkutano Mkuu wa Kanisa la TAG mwezi Agosti 1982. Hivyo mwaka huo huo Halmashauri Kuu ilifanya maamuzi ya kumteuwa Mmishenari James Ferrer kuchukua nafasi ya Mkuu wa Chuo badala ya Mmishenari Hagemeier na kukifunga Chuo kwa muda.

Chuo kilifungwa kwa mwaka mmoja tu na baadaye kikafunguliwa na kuendelea na mafunzo kama kawaida. Tangu mwaka 1983 Chuo kiliendelea kukua na kustawi na kuongezeka katika idadi ya wanafunzi, walimu na hata majengo. Mpaka sasa zaidi ya watumishi 980 wamehitimu na kuingia kwenye huduma.