TAG

Historia ya Idara ya Elimu

Idara ya Elimu ni mojawapo ya Idara kumi za Kanisa la Tanzania Assemblies of God, iliyoanzishwa kwa ajili ya kufanikisha maono na malengo yake.  Kusudi la kuwepo kwa Idara ni kupanga, kuratibu, na kusimamia utekelezaji ili kuwa na watumishi waliondaliwa vema kiroho na kitaaluma, wenye kuakisi tabia na mtazamo wa Yesu katika maisha na huduma. Idara inatoa mafunzo kwa watumishi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God na Madhehebu mbalimbali ya Kipentekoste tunayokubaliana nayo kiimani ndani na nje ya nchi.

Idara ya Elimu ina vyuo vya Biblia vinane. Vyuo vya bweni sita, kimoja cha kutwa na kimoja huria. Ili kuharakisha kazi ya kuivuna Tanzania, Uongozi wa Kanisa la TAG umeigawa Tanzania katika Kanda saba. Kila Kanda ina Chuo Mama kama ifuatavyo: Kanda ya Kusini Mashariki South-Eastern Bible College, Mtama, Lindi. Kanda ya Kusini Southern Bible College, Mbeya. Kanda ya Kati Central Bible Collge, Dodoma. Kanda ya Ziwa Lake Victoria Bible College, Mwanza. Kanda ya Kaskazini Northern Bible College, Arusha. Kanda ya Magharibi Western Bible College, Ilolanguru, Tabora. Kanda ya Kaskazini Mashariki Global Harvest Bible College, Dar–es–Salaam, na Global University ambacho kinaendesha mafunzo yake nchi nzima.

Kanisa la Tanzania Assemblies of God lilipoanza mwaka 1939 halikuwa na chuo chochote cha Biblia wala mafunzo yoyote rasmi ya kuwaandaa watumishi. Wamishenari walihubiri Injili na watu wakaokoka. Miongoni mwa hao waliookoka ambao walisikia wito wa utumishi walithibitishwa na viongozi na kuingia shambani kumvunia Bwana mavuno.

Muda sio mrefu ikaonekana kuna hitaji la kutoa Mafunzo rasmi ya kuwaandaa watumishi kwa ajili ya kulifikia taifa na Injili ya Bwana Yesu Kristo. Ndipo jitihada za kuanzisha Chuo cha Biblia zikafanyika kwa lengo la kuongeza kasi ya wimbi la uamsho. Jitihada hizo zilipelekea kuanzishwa kwa Chuo cha kwanza cha Biblia kusini mwa Tanganyika ambako uamsho ulianzia.

Mmishenari Wesley Hurst alifanya kazi ya kuweka msingi wa kuanzishwa kwa vyuo vya Biblia kwa kuanzisha vituo vya kujifunzia Neno la Mungu mkoani Mbeya mwaka 1952, juhudi ambazo zimepelekea mwaka 1954 kuzaliwa kwa Chuo cha Biblia Itende Mbeya.

Baadaye vyuo vya Biblia vya Arusha na Dodoma vilianzishwa. Kusudi kuu la kuanzishwa vyuo lilikuwa ni kuleta uamsho na kusukuma kwa haraka mpango wa kuwafikia wenye dhambi na Injili ya Yesu Kristo. Vyuo hivyo vilianzishwa kimkakati ili kuleta hamasa ya uamsho na hivyo kupenyeza Injili kwa haraka zaidi.

Mchungaji Emanuel Lazaro, Askofu Mkuu wa kwanza aliyekuwa na Mamlaka kamili, alisema kuwa kuanzishwa kwa Vyuo hivi vitatu na changamoto zilizoibuka ndiko kulikopelekea hitaji la kuwa na chombo maalum na uongozi thabiti wa kulea na kusimamia uendeshwaji wake. Hitaji hili lilikuwa la lazima ili kuvifanya kuwa endelevu na kutimiza kusudi la kuanzishwa kwa vyuo, yaani kuliwezesha Kanisa kutimiza malengo yake.

Shauku ya kuanzisha Idara ya Elimu katika kanisa la Tanzania Assemblies of God ilifikia kilele chake mwishoni mwa mwaka 1980. Kamati Kuu iliyoongozwa na Askofu Mkuu Emanuel Lazaro na Katibu Mkuu Solomon Mwagisa walikaa na kushauriana na wamishenari waliokuwepo wakati huo na kwa pamoja walikubaliana kuwepo Idara ya Elimu.

edu15

Askofu Emmanuel Lazaro

edu16

Mchungaji Solomoni Mwagiza

edu18

Mmishenari Mike McClaffin

edu18

Mmishenari Ron Hanson

Wamishenari waliohusika sana kwa ushauri katika uanzishwaji na kuendelea kwa Idara ya Elimu ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God ni Mike McClaffin na Ron Hanson. Wamishenari hawa walifanya kila lililowezekana kuona kuwa Idara ya Elimu inaanzishwa, inapata nguvu ya kiutendaji, na inatimiza kusudi la kuanzishwa kwake katika kutimiza malengo ya Kanisa.

Ingawa mwanzoni Idara ilianza kwa kusuasua, kwa msaada wa Mungu iliendelea kuimarika hadi hivi sasa. Hivi sasa Idara ya Elimu ina nguvu na ni mhimili muhimu wa kiutendaji katika Kanisa la TAG.

Mpaka tunapoandika historia hii, Kanisa la Tanzania Assemblies of God lina jumla ya vyuo vya Biblia vya bweni sita, cha kutwa kimoja, na chuo huria kimoja. Chuo cha Biblia Mbeya kilianzishwa mwaka 1954, Arusha 1958, Dodoma 1978, Mwanza 2001, Global Harvest 2009, Mtama 2010 na Western Bible College Tabora 2018. Chuo huria cha Global University kinachotoa masomo kwa masafa marefu kilianza mwaka 1972.

Tunamshukuru sana Mungu aliyeweka maono na mzigo ndani ya wamishenari na viongozi wa Kanisa kuanzisha vyuo vya Biblia ambavyo vimepelekea kuundwa kwa Idara ya Elimu. Kulingana na maelezo ya aliyekuwa Askofu Mkuu wakati huo, Mchungaji Emanuel Lazaro, wazo la kuanzisha Idara ya Elimu lilikuja baada ya Kanisa kufanikiwa kuanzisha vyuo vitatu vya kwanza vya Biblia hapa nchini ambavyo ni Mbeya, Arusha na Dodoma.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980, Idara ya Elimu imekuwa mhimili muhimu sana kwa ustawi wa Kanisa kwa kuwaandaa watumishi ambao wamefanyika baraka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Historia hii itaonesha mchango wa Idara katika kukua na kustawi kwa kanisa la Tanzania Assemblies of God kwa heshima, sifa na utukufu wa Mungu aliyewezesha uanzishwaji na mafanikio hayo.